Katika siku ya tatu ya vikao vya kujadili swala la kuundwa kwa sera ya kumlinda mtoto wa kaunti ya Kilifi, Waziri wa biashara,utalii na vyama vya ushirika,Mheshimiwa Clara Chonga,aliongoza maafisa wakuu katika serikali ya kaunti ya washikadau wengine na kujadili kwa kina kuhusu sera hiyo.
Sera hii,endapo itapitishwa na bunge la kaunti ya Kilifi, itaashiria mwanzo mpya katika harakati za kuwalinda watoto wa Kilifi dhidi ya visa vya dhulma za kijinsia, dhulma za kingono na aina yoyote ya maovu yanayofanyiwa watoto katika jamii.
Kupitia shirika la Catholic Relief Services(CRS)kupitia mpango wa “Changing the Way We Care “(CTWWC), vikao hivi ni muhimu katika kuhakikisha kwamba sheria hii inapigwa msasa kwa kuzingatia vipengee vyote muhimu vinavyowalinda watoto. Idara mbali mbali za serikali ya kaunti ya ile ya kitaifa,zimekuwa katika mstari wa mbele wa kuhakikisha sera hii itamsaidia mtoto wa Kilifi ipasavyo.